MASOMO YA MISA 13/05/2025

JUMANNE JUMA LA 4 PASAKA

MASOMO


SOMO: 1

Mdo.11:19-26
Siku zile, wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.


WIMBO WA KATIKATI: Zab.87:1-7(K)Zab.117:1
1. Msingi wake upo Juu ya milima mitakatifu.
Bwana ayapenda malango ya Sayuni Kuliko maskani zote za Yakobo.
Umetajwa kwa mambo matukufu, Ee Mji wa Mungu.

(K) Enyi mataifa yote msifuni Bwana.

2. Nitataja Rahabu na Babeli Miongoni mwao wanaonijua.
Tazama Filisti, na Tiro, na Kushi; Huyu alizaliwa humo.
Naam, mintarafu Sayuni itasemwa,
Huyu na huyu alizaliwa humo.
Na Yeye Aliye juu Ataufanya imara. (K)

3. Bwana atahesabu, awaandikapo mataifa,
Huyu alizaliwa humo.
Waimbao na wachezao na waseme,
Visima vyangu vyote vimo mwako. (K)


SHANGILIO: Yn.10:14
Aleluya, aleluya,
Bwana asema:
mimi ndimi mchungaji mwema;
Nao walio wangu nawajua,
nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.


INJILI:

 Yn.10:22-30
Huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi. Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani. Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi. Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu. Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.

MAOMBI
Pamoja na madhulumu yaliyojitokeza dhidi ya Kanisa la mwanzo, neno la Mungu lilizidi kuenea hata kwa watu wa mataifa nje ya uyahudi. Tukimtumaini Mungu, neema yake itafanya kazi daima. Tuombe msaada wa Mungu tukisema:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwalinde Baba Mtakatifu F. na Kanisa lako dhidi ya wadhalimu wasiolijali Neno lako.

2. Serikali yetu ibaki na msimamo wa kuheshimu uhuru wa kuabudu miongoni mwa raia wake.

3. Sisi kama kondoo tumsikilize Mwanao, tumwamini na kumfuata yeye aliye Mchungaji wetu Mkuu.

4. Marehemu wetu wafufuliwe na wakaongeze idadi ya Kanisa shindi huko mbinguni.

Ee Baba mwema, Mwanao ameahidi kuwa wote uliompa hakuna atakayeweza kuwapokonya katika mkono wako. Utujalie sisi sote kudumu katika Kanisa lako na kuwavutia watu wote kwako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies