MASOMO YA MISA 25/05/2025

DOMINIKA 6 YA PASAKA MWAKA C 

MASOMO


ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.48:20
Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya, yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amewakomboa watu wake, aleluya!

Utukufu husemwa.

KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi, utufanye tuzisherehekee kwa upendo motomoto siku hizi za furaha tunazoadhimisha kwa heshima ya Bwana mfufuka. Utujalie, ili hayo tunayoyakumbuka katika liturujia tuyazingatie daima kwa matendo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1:
 Mdo.15:1-2,22-29
Walishuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo. Basi ikawapendeza mitume na wazee na Kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao: Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu. Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.


WIMBO WA KATIKATI: Zab.67:1-5,7 (K)3
1. Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulikane duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote.

(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Au:
Aleluya!

2. Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K)

3. Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)


SOMO 2:
 Ufu.21:10-14,22-23
Mimi Yohane, nilichukuliwa katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, na malaika akanionesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; wenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili, na katika ile milango malaika kumi na wawili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili wa Mwanakondoo. Nami sikuona hekalu ndani yake, kwa maana Bwana Mungu Mwenyezi na Mwanakondoo, ndio hekalu lake. Na mji ule hauhitaji jua wala mwezi kuuangaza, kwa maana utukufu wa Mungu huutia nuru, na taa yake ni Mwanakondoo.


SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Yesu alisema:
Mtu akinipenda, atalishika neno langu;
na Baba yangu atampenda;
nasi tutakuja kwake.
Aleluya!


INJILI: 
Yn.14:23-29
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu zangu wapendwa, kushika amri za Yesu kunatuunganisha na Mungu Baba kwa namna ya pekee kabisa. Nguvu zote zitashindwa kututenga na upendo wa Mungu Baba.

Kwa moyo wa shukrani tuombe,
1. Bwana Yesu, ulisema: Mkishika neno langu, tutakuja kwenu na kufanya makao yetu kwenu. Utuunganishe na Mungu Baba na wenzetu kwa njia ya neno lako.

2. Utusaidie tutegemee ushirikiano na Mungu zaidi kuliko mivuto ya kidunia.

3. Kwa kuunganika na Mungu hatuwezi kupotea kwa kuwa Roho Mtakatifu anatukumbusha yote na kutuhimiza kufuata madokezo yake. Ufungue mioyo yetu tusikie sauti ya Roho Mtakatifu katika sauti zilizopo katika mahangaiko na michakato ya maisha hapa duniani.

4. Roho Mtakatifu anatujalia amani ya pekee inayotoka kwako. Utujalie kuonja amani hiyo ndani yetu na katika maisha yetu kuwashirikisha wengine walio katika mazingira yetu.

Ee Mungu Baba, tunatambua kwamba tutafanikiwa katika maisha yetu ikiwa tunaunganika nawe daima. Roho Mtakatifu aliye msaidizi wa Bwana wetu Yesu atuunganishe nawe. Upokee maombi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo anayeishi na kutawala pamoja nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu daima na milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, zipae kwako sala zetu pamoja na dhabihu tunayokutolea, ili, tukiisha kutakaswa kwa upendo wako, tuwe tunastahili kuzipokea sakramenti za huruma yako kuu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.14:15-16
Bwana asema: Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu mwenyezi wa milele, unayetutengeneza upya kwa uzima wa milele katika ufufuko wa Kristo, uzidishe kwetu tunda la sakramenti ya kipasaka, na ututilie moyoni nguvu ya chakula hiki cha wokovu. Kwa njia ya Kristo bwana wetu.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies