MASOMO YA MISA 5/06/2025

ALHAMISI JUMA LA 7 PASAKA

MASOMO

SOMO:1
 Mdo.22:30;23:6-11
Wakati ule, Jemadari alitaka kujua hakika, ni kwa sababu gani Paulo ameshitakiwa na Wayahudi, akamfungua, akawaamuru wakuu wa makuhani na baraza yote wakutane. Akamleta Paulo chini, akamweka mbele yao. Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu. Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana. Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote. Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini? Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome. Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako. Hilo ndilo neno la Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.16:1-2,7-11(K)1
1. Mungu unihifadhi mimi,
kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu,
sina wema ila utokao kwako.

(K) Mungu unihifadhi mimi,
kwa maana nakukimbilia Wewe.
Au:
Aleluya.

2. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)

3. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)

4. Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume
Mna mema ya milele. (K)

SHANGILIO: Yn.16:28
Aleluya, aleluya,
Nalitoka kwa Baba,
nami nimekuja hapa ulimwenguni;
tena nauacha ulimwengu, nakwenda kwa Baba.
Aleluya.

INJILI:
 Yn.17:20-26
Siku ile, Yesu alisali akisema: Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi. Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu. Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma. Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.

MAOMBI
Ee Roho Mtakatifu uliyeahidiwa na Bwana wetu Yesu Kristo kabla ya kupaa kwake mbinguni kwa Baba, na uliyewajia zamani mitume kule chumbani, twakuomba:

Kiitikio: Roho Mtukufu, utusikie.
1. Wewe ni Mwalimu mkunjufu unayetufundisha utakatifu, pamoja nawe hatutakosa imani tunapokaa Kanisani. Nuru yako idumu daima ndani ya Kanisa lako.

2. Ewe Chemchemi ya mapaji yote, utushushie hekima ili tukupende daima; na utujalie akili tuifahamu imani.

3. Ndiwe mwezaji wa yote, utusaidie kwa shauri tupate kupambanua mambo na kuchagua vizuri. Utujalie na nguvu, tupate kupambana na shetani kwa uhodari.

4. Utujaze elimu na mafundisho ya imani. Utuwashie moyo wa ibada na uchaji wa Mungu.

Ee Mungu, umefundisha mioyo ya waamini kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu. Utujalie katika Roho huyo kutambua na kupendelea mema na kufurahia daima faraja yake. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina.



No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies