MASOMO YA MISA 7/06/2025

JUMAMOSI JUMA LA 7 PASAKA

MASOMO

SOMO:1
 Mdo.28:16-20,30-31
Tulipoingia Rumi Paulo alipewa ruhusa kukaa kwake mwenyewe pamoja na askari aliyemlinda. Ikawa baada ya siku tatu akawaita wakuu wa Wayahudi wakutane; hata walipokutanika akawaambia, Ndugu zangu, ingawa sikufanya neno kinyume cha watu wetu wala neno lililopingamana na desturi za baba zetu, nalitiwa katika mikono ya Warumi, hali nimefungwa, tokea Yerusalemu. Na hao walipokwisha kuniuliza-uliza walitaka kunifungua, kwa maana hapakuwa na sababu yo yote kwangu ya kuuawa. Lakini Wayahudi walipotoa hoja juu ya shauri hili nalishurutishwa kutaka rufani kwa Kaisari. Si kwamba nalikuwa na neno la kuwashitaki watu wa taifa langu. Basi kwa ajili ya hayo, nimewaita mje kunitazama na kusema nami; kwa maana nimefungwa kwa mnyororo huu kwa ajili ya tumaini la Israeli. Akakaa muda wa miaka miwlli mizima katika nyumba yake aliyokuwa ameipanga, akawakaribisha watu wote waliokuwa wakimwendea, akihubiri habari za ufalme wa Mungu, na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo, kwa ujasiri mwingi, asikatazwe na mtu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.11:4-5,7(K)7
1. Bwana yu katika hekalu lake takatifu.
Bwana ambaye kiti chake kiko mbinguni,
Macho yake yanaangalia;
Kope zake zinawajaribu wanadamu.

(K) Wanyofu wa moyo wauona uso wake, Ee Bwana.
Au:
Aleluya.

2. Bwana humjaribu mwenye haki;
Bali nafsi yake humchukia asiye haki,
Na mwenye kupenda udhalimu. (K)

3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki,
Apenda matendo ya haki,
Wanyofu wa moyo watamwona uso wake. (K)


SHANGILIO: Mt.28:19-20
Aleluya, aleluya,
Enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi.
Mimi nipo pamoja nanyi siku zote,
Hata ukamilifu wa dahari.
Aleluya.

INJILI:
 Yn.21:20-25
Petro aligeuka akamwona yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata; (ndiye huyo aliyeegama kifuani pake wakati wa kula chakula cha jioni, akasema, Bwana, ni nani akusalitiye?). Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu je? Yesu akamwambia, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate mimi. Basi neno hilo lilienea katikati ya ndugu ya kwamba mwanafunzi yule hafi. Walakini Yesu hakumwambia ya kwamba hafi; bali, Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Huyu ndiye yule mwanafunzi ayashuhudiaye haya, na aliyeyaandika haya; nasi twajua ya kuwa ushuhuda wake ni kweli. Kuna na mambo mengine mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa.

MAOMBI
Ndugu, Roho Mtakatifu ni nafsi ya tatu ya Utatu Mtakatifu. Ndani yetu ametenda mema na maajabu mengi. Tumwombe ili ujio wake uimarishe hayo ambayo pamoja na Baba na Mwana ameyaanzisha ndani yetu.

Kiitikio: Mungu Roho Mtakatifu, njoo kwetu.
1. Ewe Roho Mkuu, Kipaji cha aliye juu na Kisima cha ukamilifu, utujie na kutakasa roho zetu.

2. Ee Mgeni mzuri, karibu utuletee faraja na nguvu tele.

3. Ewe dawa ya vidonda vyote, njoo uziangaze nyoyo zetu na ufute makovu yote.

4. Bila wewe hatuwezi kutenda jema lolote kwani tu dhaifu, tafadhali utujie na mapaji yako saba.

Ee Mungu, umefundisha mioyo ya waamini kwa mwangaza wa Roho Mtakatifu. Utujalie katika Roho huyo kutambua na kupendelea mema na kufurahia daima faraja yake. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo, Bwana wetu. Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies