MASOMO YA MISA 25/06/2025

JUMATANO JUMA 12 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.15:1-12,17-18
Neno la Bwana likamjia Abrahamu katika njozi, likinena, Usiogope Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abrahamu akasema, Ee Bwana Mungu, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi ili uirithi. Akasema, Ee Bwana Mungu nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, Na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akawaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:1-4,6-9 (K)8
1. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, Wajulisheni watu matendo yake, Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote.

(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.

2. Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote. (K)

3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Ibrahimu, uapo wake kwa Isaka. (K)

SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, ee Yerusalemu,
huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!

INJILI:
 Mt.7:15-20
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuza matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.

MAOMBI
Ndugu, huku tukikumbuka kuwa sisi ni kama miti ya matunda, tuombe msaada wa Mungu tukisema:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa kumhubiri Kristo Mwanao kwa ufasaha, ili watu wako wasitekwe na manabii wa uwongo. Ee Bwana.

2. Uamshe mioyo ya watawala wa dunia wasiolitukuza jina lako, ili wayashike maagizo yako, na shuhuda zako, na amri zako kwa moyo wote na kwa roho yote. Ee Bwana.

3. Kwa kuwa umetupatia sisi na vizazi vijavyo nchi hii iwe milki yetu pindi tupo hapa duniani, utujalie kuzitumia mali zetu kwa sifa na utukufu wako. Ee Bwana.

4. Umjalie kila mmoja wetu kuzaa matunda mema yaletayo uzima wa milele. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wafikishwe kwenye nchi uliyotuahidia huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tuzae matunda yatakayodumu mpaka uzima wa milele, utujalie hayo tuliyokuomba. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies