MASOMO YA MISA 16/05/2025

IJUMAA JUMA LA 4 PASAKAMASOMO

SOMO:1
 Mdo.13:26-33
Paulo alisimama akawapungia mkono akasema: Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa. Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu. Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe. Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini. Lakini Mungu akamfufua katika wafu; akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu. Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa, ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.


WIMBO WA KATIKATI: Zab.2:6-11(K)7
1. Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni,
mlima wangu mtakatifu.
Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

(K) Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

2. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
Utawaponda kwa fimbo ya chuma,
Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. (K)

3. Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
Mtumikieni Bwana kwa kicho,
Shangilieni kwa kutetemeka. (K)


SHANGILIO: Rum.6:9
Aleluya, aleluya,
Wewe Toma, umesadiki kwa kuwa umeniona,
wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.


INJILI: 
Yn.6:52-59
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo. Nami niendako mwaijua njia. Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia? Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.

MAOMBI
Mungu alimfufua Yesu Kristo katika wafu, naye akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemnu. Kwa kuwa sasa yu kati yetu, na sisi ndio mashahidi wake mbele ya watu, tuombe:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wa Kanisa wasichoke kusimama mbele ya watu na kulihubiri neno lako.

2. Tunawaombea watawala wa dunia, ili wazilinde sheria nzuri zilizotungwa; pia wadumishe haki, amani na usawa.

3. Sisi sote tunaomwamini Mungu tuondolewe au tukingwe na fadhaa yoyote mioyoni mwetu.

4. Maneno haya ya Zaburi ya pili: “Wewe ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa," na yasikike leo kwa kila ndugu yetu marehemu.

Ee Mungu, Mwanao ndiye njia, ukweli, na uzima; na hakuna mtu atakayefika kwako bila kupitia kwake. Basi, uyapokee maombi yetu kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies