MASOMO YA MISA 17/05/2025

JUMAMOSI JUMA LA 4 PASAKAMASOMO

SOMO:1
 Mdo.13:44-52
Paulo na wenziwe waliingia katika sinagoni siku ya sabato, wakaketi. Watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu. Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.


WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-4(K)3
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.

(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.

2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)

3. Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)


SHANGILIO: Rum. 6:9
Aleluya, aleluya,
Kristo akiisha kufufuka katika wafu,
hafi tena wala mauti haimtawali tena.
Aleluya.


INJILI:
 Yn.14:7-14
Yesu aliwambia wanafunzi wake: Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

MAOMBI
Wapendwa katika Kristo, sisi sote tuliobatizwa tumeamriwa na kuwekwa na Bwana kuwa nuru ya mataifa, tupate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Hata hivyo, twahitaji msaada wake. Tuombe:

Kiitikio: Mungu wa huruma utusikie.
1. Wahubiri wote wa neno lako wapokelewe kwa furaha popote linapohitajika neno hilo la wokovu.

2. Wote wenye madaraka katika jamii waonje furaha ya kustahilishwa uzima wa milele kwa njia ya huduma bora wanazotoa kwa watu wako.

3. Utuepushe na wivu, ubishi wa bure na matukano yanayofifisha nuru ya upendo aliotuletea Mwanao.

4. Marehemu wetu waliokuona, hata kwa jicho la imani tu; au kukusikia, hata kwa sikio la imani tu, sasa waonane nawe uso kwa uso.

Ee Mungu Mwema, Mwanao ametuahidi kuwa tukiomba lolote kwa jina lake atalifanya. Basi, uipokee sala yetu kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina. 

No comments

Post a Comment

Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies