MASOMO YA MISA 12/07/2025

JUMAMOSI JUMA 14 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1:
 Mwa.49:29-33;50:15-25
Yakobo aliwaamuru wanawe: Mimi ninakwenda kukusanywa pamoja na watu wangu; mnizike pamoja na baba zangu, katika pango iliyomo shambani mwa Efroni, Mhiti; katika ile pango iliyomo shambani mwa Makpela, iliyo mbele ya Mamre katika nchi ya Kanaani, aliyoinunua Ibrahimu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake pa kuzikia. Humo walimzika Ibrahimu, na Sara mkewe; humo wakamzika Isaka, na Rebeka mkewe; nami humo nikamzika Lea; shamba na pango iliyomo lililonunuliwa kwa bani Hethi. Basi Yakobo alipokwisha kuwaagiza wanawe, akakunja miguu yake kitandani, akafa, akakusanywa pamoja na watu wake. Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; nave atatulipa maovu yetu tuliyomtenda. Wakapeleka watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema, Mwambieni Yusufu hivi, Nakuomba uwaachilie ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utuachilie kosa la watumwa wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye. Nduguze wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumwa wako. Yusufu akawaambia, Msiogope, je! mimi ni badala ya Mungu? Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo. Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha, na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema. Akakaa Yusufu katika Misri, yeye na nyumba ya babaye. Akaishi lusuru miaka mia na kumi. Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu. Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha kutoka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akisema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:1-4,6-7 (K)Zab.69:32
1. Aleluya. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, Wajulisheni watu matendo yake, Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote.

(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.

2. Jisifuni kwa jina lake lakatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake siku zote. (K)

3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo wateule wake. Yeye Bwana, ndiye Mungu wetu, duniani mwote mna hukumu zake. (K)

SHANGILIO: 1Pet.1:25
Aleluya, aleluya!
Neno la Bwana hudumu hata milele,
na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya!

INJILI:
 Mt.10:24–33
Yesu aliwafundisha mitume wake: Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake. Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake? Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana. Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi. Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

MAOMBI
Ndugu, tunao wajibu mkubwa kwa Mungu na kwa jirani zetu huku imani yetu ikiwa katika upinzani. Tumwombe Mungu kupitia Mama yetu Bikira Maria tukisema:-

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F., Maaskofu na viongozi wote wa Kanisa waongezewe ujasiri katika kufundisha imani sahihi, kuilinda na kuitetea bila woga wowote. Ee Bwana.

2. Uwajalie viongozi wa dunia kukumbuka daima, kwamba wanawaongoza watu kwa dhamana yako Wewe, uliye Bwana wa majeshi na Mungu Mtakatifu. Ee Bwana.

3. Waongoe ndugu zetu wanaomkana Mwanao Yesu Kristo, ili naye asije kuwakana mbele yako huko mbinguni. Ee Bwana.

4. Uamshe ndani ya kila mmoja wetu tabia ya uwazi na ukweli; na hivi kuondoa hofu, masengenyo na hali ya kudhaniana vibaya. Ee Bwana.

5. Kwa rehema yako, uwapokee kwako mbinguni ndugu zetu marehemu. Ee Bwana.

Ee Mungu Baba, Mwanao alisema: “Si ninyi msemao bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.” Uipokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 11/07/2025

IJUMAA JUMA 14 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1:
 Mwa.46:1-7,28-30
Israeli alisafiri pamoja na yote aliyokuwa nayo, akaja Beer-sheba, akamchinjia sadaka Mungu wa Isaka babaye. Mungu akanena na Israeli katika ndoto ya usiku, akasema, Yakobo, Yakobo. Akasema, Mimi hapa. Akasema, Mimi ni Mungu, Mungu wa baba yako, usiogope kushuka mpaka Misri; maana nitakufanya uwe taifa kubwa huko. Mimi nitashuka pamoja nawe mpaka Misri; nami nitakupandisha lena bila shaka; na Yusufu ataweka mkono wake juu ya macho yako. Yakobo akaondoka kutoka Beer-sheba; wana wa Israeli wakamchukua baba yao, na watoto wao wadogo, na wake zao katika magari aliyoyapeleka Farao ili kumchukua. Wakatwaa na wanyama wao, na mali zao walizokuwa wamezipata katika nchi ya Kanaani, wakaja Misri, Yakobo na uzao wake wote pamoja naye. Wanawe, na wana wa wanawe, pamoja naye, binti zake na binti za wanawe, na uzao wake wote, aliwaleta pamoja naye mpaka Misri. Yakobo akampeleka Yuda mbele yake kwa Yusufu, ili amwongoze njia mpaka Gosheni. Wakaja mpaka nchi ya Gosheni. Yusufu akatandika gari lake, akapanda kwenda kumlaki Israeli, babaye, huko Gosheni; akajionyesha kwake, akamwangukia shingoni, akalia shingoni mwake, kitambo kizima. Israeli akamwambia Yusufu, Na nife sasa, kwa kuwa nimekuona uso wako, ya kuwa ungali hai.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.37:3-4,18-19,27-28,39-40 (K)39
1. Umtumaini Bwana ukatende mema, ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. Nawe utajifurahisha kwa Bwana, naye atakupa haja za moyo wako.

(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana.

2. Bwana anazijua siku za wakamilifu, na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, na siku za njaa watashiba. (K)

3. Jiepue na uovu, utende mema, na kukaa hata milele. Kwa kuwa Bwana hupenda haki, wala hawaachi watauwa wake. (K)

4. Na wokovu wenye haki una Bwana, Yeye ni ngome yao wakati wa taabu. Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa, huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa, kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)

SHANGILIO: Yak.1:21
Aleluya, aleluya!
Pokeeni kwa upole neno la Mungu
lililopandwa ndani,
liwezalo kuziokoa roho zenu.
Aleluya!

INJILI: 
Mt.10:16-23
Yesu aliwaambia mitume wake: Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

MAOMBI
Ndugu, maisha ni safari yenye hatari nyingi. Kwa vile sisi ni wasafiri tunaohitaji msaada wa Mungu, tuombe.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Viongozi wa Kanisa wajaliwe ujasiri wa kunena na kutenda matendo yako makuu, kwa nguvu ya Roho wako Mtakatifu, dhidi ya maadui wa imani yetu. Ee Bwana.

2. Watawala wa dunia waheshimu uhuru wa dini na kuwachukulia hatua za kisheria wote wanaovuruga amani na kukiuka haki za binadamu. Ee Bwana.

3. Utuondolee maovu yote; na daima utukumbushe kuwa njia zako zimenyooka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake. Ee Bwana.

4. Utuepushe na usaliti; aidha utujalie upendo wa kweli na ari ya kuwa tayari kuteswa, kwa ajili ya kutangaza Injili yako popote ulimwenguni. Ee Bwana.

5. Wagonjwa wetu wajaliwe uvumilivu na afya njema; na marehemu wetu wapokelewe katika makao yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyezisikiliza sala za Mwanao hata alipokuwa msalabani, uzipokee sala zetu katika adhimisho hili. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 10/07/2025

ALHAMISI JUMA 14 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1:
 Mwa.44:18-21,23-29;45:1-5
Yuda alimkaribia Yusufu akasema, Tafadhali, bwana wangu, mtumwa wako na aseme neno moja masikioni mwa bwana wangu, wala hasira yako isimwakie mtumwa wako, maana wewe u kama Farao. Wewe, bwana wangu ulituuliza watumwa wako, ukisema, Je! mnaye baba, au ndugu? Tukakuambia wewe, bwana wangu, Tunaye baba, naye ni mzee, na mwana wa uzee wake ni mdogo, na nduguye amekufa; amebaki yeye peke yake wa katika tumbo la mamaye, na baba yake anampenda. Ukatuambia watumwa wako, Mleteni kwangu, ili macho yangu yamwangalie. Asiposhuka ndugu yenu mdogo pamoja nanyi, hamtaniona uso wangu tena. Ikawa tulipokwenda kwa mtumwa wako, baba yangu, tukamwarifu maneno yako, bwana wangu. Kisha baba yetu akanena, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. Tukasema, Hatuwezi kwenda; ndugu yetu mdogo akiwapo pamoja nasi, tutashuka; maana hatutaweza kuuona uso wa mtu huyo, ndugu yetu mdogo asipokuwa pamoja nasi. Mtumwa wako, Baba yangu, akatuambia, Mnajua ya kuwa mke wangu alimzalia wana wawili; mmoja alitoka kwangu, nikasema, Bila shaka ameraruliwa, wala sikumwona tangu hapo. Na mkiniondolea huyu naye, na madhara yakimpata, mtashusha mvi zangu na msiba kaburini. Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema. mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha za watu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:16-21 (K)5
1. Bwana aliita njaa iijilie nchi, akakiharibu chakula chote walichokitegemea. Alimpeleka mtu mbele yao, Yusufu aliuzwa utumwani.

(K) Zikumbukeni ajabu Bwana alizozifanya.

2. Walimwumiza miguu yake kwa pingu, Akatiwa katika minyororo ya chuma. Hata wakati wa kuwadia neno lake, Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)

3. Mfalme alituma watu akamfungua, Mkuu wa watu akamwachia. Akamweka kuwa Bwana wa nyumba yake, Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

SHANGILIO: Ebr.4:12
Aleluya, aleluya!
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu,
li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya!

INJILI: 
Mt.10:7-15
Yesu aliwaambia mitume wake: Katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake. Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka. Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni. Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi. Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu. Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.

MAOMBI
Ndugu, Mungu anazo njia nyingi za kuufanikisha mpango wake wa ukombozi. Kwa imani na matumaini, tumwombe.

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umjalie Askofu wetu F. uvumilivu katika kuzikabili changamoto za sasa za kitume kwa ajili ya ustawi wa jimbo letu. Ee Bwana.


2. Watawala wa dunia wayatumie vyema madaraka yao, ili kujenga jamii zenye haki, amani na upendo wa kweli. Ee Bwana.

3. Utujalie sisi sote kutimiza wajibu zetu za kitume kwa ujasiri na bila kutarajia malipo yoyote hapa duniani. Ee Bwana.

4. Kwa huruma yako, patiliza ukali wa hasira yako kwa wakosefu, maana Wewe ndiwe Mtakatifu katikati yetu. Ee Bwana.

5. Uwapoze wagonjwa wetu, uwatakase wenye ukoma, uwafukuze pepo wabaya na kuwafufua wafu kwa uzima wa milele. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetujia kwa namna ya pekee kila tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 9/07/2025

JUMATANO JUMA 14 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.41:55-57;42:5-7,17-24
Nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote. Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani. Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake. Yusufu akawaona nduguze akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema, Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula. Akawatia wote gerezani siku tatu. Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. Kama ni wa kweli ninyi, ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia; kwa hiyo shida hii imetupata. Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao. Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:1-2,10-11,18-19 (K)22
1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo. Mshukuruni Bwana kwa kinubi, Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.

(K) Ee Bwana fadhili zako zikae nasi,
kama vile tulivyokungoja Wewe.

2. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa, huyatangua makusudi ya watu. Shauri la Bwana lasimama milele, makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. (K)

3. Tazama jicho la Bwana li kwa wamchao Wazingojeao fadhili zake. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

SHANGILIO: Kol.3:16,17
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo likae kwa wingi
ndani yenu katika hekima yote,
mkishukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya!

INJILI:
 Mt.10:1-7
Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema. Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

MAOMBI
Ndugu, kwa Ubatizo sisi sote tumeitikia wito wa kuwa watangazaji wa Injili. Kwa vile sisi ni viumbe dhaifu na kazi hiyo si rahisi hivi, tuombe msaada wa Mungu tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie. 1. Upende kumlinda Askofu wetu F. na wote uliowateua kuirithi kazi ya mitume. Ee Bwana.

2. Ubariki juhudi za viongozi wetu wa serikali na wa taasisi mbalimbali katika kutafuta ufumbuzi wa mata- tizo ya njaa, ajira na yote yanayozikera jamii zetu. Ee Bwana.

3. Watu wote duniani watambue kuwa sasa wakati umewadia wa kukutafuta Wewe, hata utakapokuja na kuwanyeshea haki. Ee Bwana.

4. Kila mmoja wetu aitikie kwa vitendo wito wa kuwa mtangazaji wa msamaha, upendo wa kidugu na Habari Njema ya wokovu kwa watu wote. Ee Bwana.

5. Ufalme wako uwafikie kwa namna ya pekee ndugu zetu marehemu tuliowapenda na kuwategemea kimwili na kiroho. Ee Bwana.

Ee Mungu unayewapa watu wako mahitaji ya kimwili na kiroho kwa namna ya ajabu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 8/07/2025

JUMANNE JUMA 14 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1:
 Mwa.32:23-33
Yakobo aliondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo. Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusu panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye. Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n’nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko. Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi vangu imeokoka. Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake. Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.17:1-3,6-8,15 (K)15
1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.

(K) Nikutazame uso wako katika haki.

2. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose. (K)

3. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu, Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea. (K)

4. Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako; mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)


SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu,
nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!

INJILI:
 
Mt.9:32-39
Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wowote. Lakini Mafarisayo wakasema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo. Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apelike watenda kazi katika mavuno yake.

MAOMBI
Ndugu, pamoja na uhodari wao, malaika wanalishika neno la Mungu. Nasi tuombe neema yake Mungu tukisema.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Baba Mtakatifu F. na viongozi wote wa Kanisa lako uhodari, katika kuzikabili changamoto zote zinazolikumba Kanisa katika ulimwengu wa sasa. Ee Bwana.

2. Uwaonye walimwengu wanaodiriki kulikufuru jina lako na uwaongoe, ili waanze maisha mapya yenye imani katika nguvu yako kuu dhidi ya dhambi, shetani na mauti. Ee Bwana.

3. Uwajalie vijana wengi kuitikia wito wako kila siku; na wale uliokwisha wateua kuwa watangazaji wa Injili yako, wadumu kiaminifu katika utume huo. Ee Bwana.

4. Utujalie kuzitumia fedha na raslimali zetu kulijenga Kanisa na kulitukuza jina lako; na siyo kusababisha machafuko au maabudu ya sanamu. Ee Bwana.

5. Uwapokee ndugu zetu marehemu kwenye makao yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu, pamoja na malaika wako twayaleta maombi yetu kwako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.





MASOMO YA MISA 7/07/2025

JUMATATU JUMA 14 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.28:10-22
Yakobo alitoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulanl akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamisha juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama. malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli, Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu. Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililosimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.91:1-4,14-15 (K)2
1. Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.

(K) Mungu wangu nitakayemtumaini.

2. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. (K)

3. Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua jina langu. Ataniita nami nilamwitikia; NitaKuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza. (K)

SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao,
hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya!

INJILI:
 Mk1:14-20
Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu, Imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.

MAOMBI
Ee Mungu, Wewe ni mwaminifu katika ahadi zako; na akuombaye kwa imani hakosi kupata thawabu yake. Kwa hiyo twakuomba.

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F., na Wakleri wote wadumu kiaminifu katika kuwafundisha waamini uliowaposa wawe wako kwa milele; ili wakujue Wewe. Ee Bwana.

2. Kwa huruma yako, uendeleze miujiza yako katika Kanisa na dunia nzima ya leo inayozidi kuonewa na ibilisi. Ee Bwana.

3. Serikali yetu itoe kipaumbele katika huduma za afya; na uzikinge jamii zetu na imani potofu dhidi ya vifo na magonjwa. Ee Bwana.

4. Utumiminie baraka zako na kumjalia kila mmoja wetu kukutegemea Wewe Mungu katika taabu na raha. Ee Bwana.

5. Wagonjwa wetu wapone na wafu wafufuliwe na kushiriki uzima mpya. Ee Bwana.

Ee Mungu unayemjazi kila anayekujia kwa imani na matumaini, uipokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.











MASOMO YA MISA 6/07/2025

DOMINIKA YA 14 MWAKA C

MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.48:9-10
Tumezitafakari fadhili zako, ee Mungu, katikati ya hekalu lako. Kama lilivyo jina lako, ee Mungu, ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia. Mkono wako wa kuume umejaa haki.

KOLEKTA:
Ee Mungu, kwa njia ya unyenyekevu wa Mwanao umeuinua ulimwengu uliokuwa umeanguka. Uwajalie waamini wako furaha takatifu ili, hao uliowaondoa katika utumwa wa dhambi, wapate kuifikia furaha ya milele. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1:
 Isa.66:10-14
Furahini pamoja na Yerusalemu, shangilieni kwa ajili yake, ninyi nyote mmpendao; furahini pamoja naye kwa furaha, ninyi nyote mliao kwa ajili yake; mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake, mpate kukama, na kufurahiwa kwa wingi wa utukufu wake. Maana Bwana asema hivi, Tazama, nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa. Mfano wa mtu ambaye mama yake amfariji, ndivyo nitakavyowafariji ninyi; nanyi mtafarijiwa katika Yerusalemu. Nanyi mtaona, na mioyo yenu itafurahi, na mifupa yenu itasitawi kama majani mabichi; na mkono wa Bwana utajulikana, uwaelekeao watumishi wake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.66:1-7,16,20,(K)1
1. Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
Imbeni utukufu wa jina lake.
Tukuzeni sifa zake,
Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini!

(K) Mpigie Mungu kelele za shangwe,
nchi yote,

2. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
Naam, italiimba jina lako.
Njoni yatazameni matendo ya Mungu,
Hutisha kwa mambo awatendayo wanadamu. (K)

3. Aligeuza bahari ikawa nchi kavu;
Katika mto walivuka kwa miguu;
Huko ndiko tuliko mfurahia,
Atawala kwa uweza wake milele. (K)

4. Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu,
Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu.
Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu,
Wala kuniondolea fadhili zake. (K)

SOMO 2: 
Gal.6:14-18
Mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu. Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya. Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu. Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.

SHANGILIO: Yn.1:12,14
Aleluya, aleluya!
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
wote waliompokea aliwapa uwezo wa
kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya!

INJILI: 
Lk.10:1-12,17-20 (au somo fupi Lk.10:1-9)
Baada ya hayo Bwana aliweka na wengine, sabini, akawatuma wawili wawili wamtangulie kwenda kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda mwenyewe. Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake. Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. Msichukue mfuko, wala mkoba, wala viatu; wala msimwamkie mtu njiani. Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihamehame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.
(10:10-12,17-20) Na mji wowote mtakaouingia, nao hawawakaribishi, tokeni humo, nanyi mkipita katika njia zake semeni, Hata mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana na miguu yetu tunayakung'uta juu yenu. Lakini jueni hili, ya kuwa Ufalme wa Mungu umekaribia. Nawaambia ya kwamba siku ile itakuwa rahisi zaidi Sodoma kuistahimili adhabu yake kuliko mji huo. Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru. Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.

MAOMBI
Bwana Yesu alitaka kuwatayarisha wasaidizi na kuwaita mitume atakaowatuma kuendeleza utume alioanzisha yeye mwenyewe. Aliwapa mitume wake maagizo mengi tuliyosikia katika Enjili ya leo. Baada ya kupaa mbinguni, Yesu aliwapelekea Roho wake ili awaimarishe kutimiza maagizo waliyopewa.

Ee Bwana Yesu,
1. Uliwapeleka mitume duniani ili watangaze habari ya Ufalme wa Mungu; uwaimarishe wote uliowachagua kwa utumishi wako.

2. Uliwaambia mitume wafuate njia uliyotangulia kuienda; utupe moyo tutegemee njia yako zaidi kuliko maarifa yetu ya kibinadamu.

3. Uliwatayarisha mitume wako waishi kadiri ya masharti ya Ufalme wa Mungu: utuwezeshe kuishi kadiri ya yale tunayoyatangaza.

4. Mitume wako walijaliwa amani wawashirikishe waumini. Utusaidie kueneza amani yako bila magomvi wala mafarakano.

5. Ulisema kwamba mti mwema unajulikana kwa matunda yake, utusaidie tuzalishe matendo mema kwa imani.

Ee Mungu Mwenyezi, uliweka mitume wawakusanye waumini wako. Uyasikilize maombi yetu tuwe waumini waaminifu kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunaomba sadaka tunayotoa kwa heshima ya jina lako itutakase, na ituwezeshe kutenda siku kwa siku kadiri ya uzima wa mbinguni. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.34:8
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; heri mtu yule anayemtumaini.

Au:
Mt.11:28
Bwana asema: Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sisi tulioshibishwa na sadaka kubwa namna hii, tunakuomba utujalie kuitunza zawadi hiyo iletayo wokovu, wala tusiache kamwe kukusifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

MASOMO YA MISA 5/07/2025

JUMAMOSI JUMA 13 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.27:1-5,15-29
Ikawa Isaka alipokuwa mzee, na macho yake yamepofuka asione, akamwita Esau, mwanawe mkubwa, akamwambia, Mwanangu. Nave akamwitikia, Mimi hapa. Akasema, Tazama, sasa mimi nimekuwa mzee, wala sijui siku ya kufa kwangu. Basi, nakuomba, chukua mata yako, podo lako na upinde wako, ukaende nyikani uniwindie mawindo; ukanifanyie chakula kitamu namna ile niipendayo, ukaniletee, ili nile; na roho yangu ikubariki, kabla sijafa. Na Rebeka akasikia, Isaka aliposema na Esau mwanawe. Basi Esau akaenda nyikani awinde mawindo, ayalete. Kisha Rebeka akatwaa mavazi mazuri ya Esau mwanawe mkubwa, aliyokuwa nayo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. Na ngozi za wana-mbuzi akamvika mikononi, na katika ulaini wa shingo yake. Naye akampa Yakobo mwanawe mikononi mwake hicho chakula kitamu na mkate alioufanya. Akaja kwa baba yake, akasema, Babangu. Akasema, Mimi hapa, U nani wewe, mwanangu? Yakobo akamwambia babaye, Mimi ni Esau, mzaliwa wako wa kwanza, nimefanya kama ulivyoniambia. Ondo- ka, tafadhali, ukae kitako, ule mawindo yangu, ili roho yako inibariki. Isaka akamwuliza mwanawe, Imekuwaje umepata upesi namna hii, mwanangu? Akasema, Kwa sababu Bwana, Mungu wako, amenifanikisha. Isaka akamwambia Yakobo, Karibu, tafadhali, ili nikupapase, mwanangu, nione kwamba wewe ndiwe mwanangu Esau, ama siyo. Basi Yakobo akamkaribia Isaka, babaye, naye akampapasa, akasema, Sauti ni sauti ya Yakobo, lakini mikono ni mikono ya Esau. Wala hakumtambua, kwa maana mikono yake ilikuwa kama mikono ya Esau, ndugu yake, yenye malaika; basi akambariki. Akamwuliza, Wewe ndiwe kweli mwanangu Esau? Akasema, Ndimi. Akasema, Niletee karibu nami nipate kula mawindo ya mwanangu, ili roho yangu ikubariki. Akamsogeza karibu, naye akala; kisha akamletea mvinyo, akanywa. Isaka, baba yak, akamwambia, Njoo karibu sasa, ukanibusu, mwanangu. Akamkaribia akambusu. Naye akasikia harufu ya mavazi yake, akambariki akasema, Tazama, harufu ya mwanangu Ni kama harufu ya shamba alilolibariki Bwana. Mungu na akupe ya umande wa mbingu, Na ya manono ya nchi, Na wingi wa nafaka na mvinyo, Mataifa na wakutumikie Na makabila wakusujudie, Uwe bwana wa ndugu zako, na wana wa mama yako na wakusujudie, atakayekulaani alaaniwe, Na atakayekubariki abarikiwe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.135:1-6 (K)3
1. Aleluya. Lisifuni jina la Bwana, Enyi watumishi wa Bwana, sifuni. Ninyi msimamao nyumbani mwa Bwana, Nyuani mwa nyumba ya Mungu wetu.

(K) Msifuni Bwana kwa kuwa ni mwema.

2. Msifuni Bwana kwa kuwa Bwana ni mwema. Liimbieni jina lake kwa maana lapendeza. Kwa sababu Bwana amejichagulia Yakobo, Na Israeli, wawe watu wake hasa. (K)

3. Maana najua ya kuwa Bwana ni mkuu. Na Bwana wetu yu juu ya miungu yote. Bwana amefanya kila lililompendeza, Katika mbingu na katika nchi, Katika bahari na katika vilindi vyote. (K)

SHANGILIO: Mt.4:4
Aleluya, aleluya!
Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno litokalo katika
kinywa cha Mungu.
Aleluya!

INJILI: 
Mt.9:14-17
Wanafunzi wake Yohane walimwendea Yesu wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga. Hakuna mtu atiaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; maana kile kilichotiwa huondoa kipande cha lile vazi, na pale palipotatuka huzidi. Wala watu hawatii divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama wakitia, vile viriba hupasuka, divai ikamwagika, na viriba vikaharibika; bali hutia divai mpya katika viriba vipya, vikahifadhika vyote.

MAOMBI
Wapendwa, njia za Mungu ni za ajabu na mipango yake haitabiriki. Kwa vile kwake yote yawezekana, kwa maombezi ya Bikira Maria, tuombe neema yake.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uzidi kulijalia Kanisa lako viongozi halali na wenye sifa zinazokubalika mbele yako. Ee Bwana.

2. Uwajalie wazazi na viongozi wote wa jumuiya zetu neema ya kutawala vionjo vyao; wawe na upendo wa kweli, na siyo ubaguzi, ili haki, amani na usawa vitawale familia na jumuiya zetu. Ee Bwana.

3. Kila mmoja wetu ajaliwe kutafuta riziki na nafasi yake katika jamii, kwa njia halali, na hivi kutimiza mapenzi yako. Ee Bwana.

4. Uwasamehe wadhambi, uwafariji wafungwa na kuwaacha huru watumwa, wapate kuishi kwa amani na raha. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wafunguliwe vifungo vyao na kushirikishwa karamu ya arusi isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Bwana Mungu, twatamani kufika kwako ambako hakuna maombolezo wala mfungo. Utujalie hayo yote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 4/07/2025

IJUMAA JUMA 13 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.23:1-4,19;24:1-8,62-67
Umri wake Sara ulikuwa miaka mia na ishirini na saba, ndio umri wake Sara. Sara akafa katika Kiriath-arba, ndio Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu akaja kumlilia Sara na kumwombolezea. Akaondoka Ibrahimu kutoka mbele ya maiti wake, akasema na bani Hethi, akinena, Mimi ni mgeni, ninatembea kwenu; nipeni mahali pa kuzikia kwenu, pawe pangu, nimzike maiti wangu atoke mbele yangu. Basi baada ya hayo Ibrahimu akamzika Sara mkewe katika pango ya shamba la Makpela kuelekea Mamre, ndiyo Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babaangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, anwe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. Basi isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana laikaa katika nchi ya kusini. Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja. Rebeka akainua macho, anaye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamaake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.106:1-5 (K)1
1. Aleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Nani awezaye kuyanena matendo makuu ya Bwana, kuzihubiri sifa zake zote.

(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.

2. Heri washikao hukumu, Na kutenda haki sikuzote. Ee Bwana, unikumbuke mimi, Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako. (K)

3. Unijilie kwa wokovu wako, Ili niuone wema wa wateule wako. Nipate kuifurahia furaha ya taifa lako, Na kujisifu pamoja na watu wako. (K)

SHANGILIO: Zab.130:5
Aleluya, aleluya!
Roho yangu inamngoja Bwana,
na Neno lake nimelitumainia.
Aleluya!

INJILI:
 Mt.9:9-13
Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata. Ikawa alipoketi nyumbani ale chakula, tazama, watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuja wakaketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi. Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.

MAOMBI
Ndugu zangu, Yesu Kristo hakuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi. Kwa vile kuitikia wito wake ni kukubali majukumu yanayoambatana na wito huo, tuombe neema yake:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kwa utii wa Mwanao aliouonesha mpaka msalabani, uwajalie viongozi wote wa Kanisa neema ya utii wa daima na udumifu katika kushika viapo vyao, walivyovifanya mbele yako na mbele ya Kanisa zima. Ee Bwana.

2. Wote wenye mamlaka watimize wajibu wao, hasa katika kusimamia haki na maadili mema kwa raia wao. Ee Bwana.

3. Wote wasiokukiri Wewe wajaliwe kutambua kuwa wanafanana na wagonjwa wasiojijua na waongoke na kupata tiba ya kiroho. Ee Bwana.

4. Utuwezeshe kuwahurumia na kuwarekebisha wakosefu; kama alivyofanya Mwanao, Yesu Kristo, apendaye rehema na siyo sadaka. Ee Bwana.

5. Uwaite marehemu wetu wapate kushiriki karamu yako isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu mpaji wa vyote, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 3/07/2025

MTAKATIFU TOMA MTUME

MASOMO

SOMO: 
Efe.2:19-22
Tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.117(K)Mk.16:15
Aleluya.
1. Enyi mataifa yote, mhimidini.
enyi watu wote, mhimidini.

(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili.

2. Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)

SHANGILIO: Yn.20:29
Aleluya, aleluya!
Wewe, Tomaso,
kwa kuwa umeniona, umesadiki,
wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya!

INJILI:
 Yn.20:24-29
Mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu Basi wanafunzi wengine wakamwambia, Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo. Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.

MAOMBI
Ndugu zangu wapendwa, Kwa maombezi ya Mitume tumwombe Kristo, Bwana wa Kanisa lake.

1. Uliwaweka mitume kuwa mashahidi wa ufufuko wako na kuwatuma duniani kote waitangaze habari hii ya furaha: Uwasaidie Baba Mtakatifu J. na maaskofu wote uliowachagua kuwa mahalifa wa mitumne wako kuliongoza kanisa lako kwa busara na hekima.

2. Uliwaagiza mitume watangaze neno lako kati ya mataifa yote: Uwajaze Roho Mtakatifu wahubiri wote wa neno lako.

3. Uliweka kanisa lako juu ya msingi wa mitume: Ulifanye Kanisa lako kuwa alama ya umoja na ya amani kati ya mataifa.

4. Uliwaagiza mitume wawaondolee dhambi wale wote wanaotubu: Uwatie moyo mpya wote wanaoungama dhambi zao.

Bwana Yesu, unastahili kupokea heshima yote, upokee shukrani na sifa katika Kanisa lako pamoja na Baba na Roho Mtakatifu sasa na siku zote daima na milele. Amina


.

MASOMO YA MISA 2/07/2025

JUMATANO JUMA 13 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.21:5,8-20
Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huko mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji yakaishaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa akimkabili, mbali i kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapazaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:6-7,9-13 (K)6
1. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, Akamwokoa na taabu zake zote. Malaika wa Bwana hufanya kituo, akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.

(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.

2. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, yaani, wamchao hawahitaji kitu. Wana-simba hutindikiwa, huona njaa, bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu chochote kilicho chema. (K)

3. Njoni, enyi wana, mnisikilize, nami nitawafundisha kumcha Bwana. Ni nani mtu yule apcndezwaye na uzima, apendaye siku nyingi apate kuona mema? (K)

SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
mungu alikuwa ndani ya Kristu,
Neno lako ni taa ya miguu yangu,
na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!

INJILI: 
Mt.8:28-34
Yesu alipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu? Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha. Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe. Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini. Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote, na habari za wale wenye pepo pia. Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao.

MAOMBI
Ndugu, si rahisi kuitekeleza amri ya mapendo kwa jirani, hasa pale zinapokuwepo tofauti baina ya wahusika, mintarafu uzao wa damu na usio wa damu. Tuombe neema ya Mungu tukisema:-

Kiitikio: Twakuomba utusikie. 1. Uwajalie Maaskofu na Mapadre wetu kushirikiana vema zaidi na watenda kazi wao, bila ubaguzi wa aina yoyote. Ee Bwana.

2. Wote wenye mamlaka wajaliwe roho ya kugawa madaraka na raslimali zilizopo, kwa njia za haki na amani bila upendeleo wowote ule. Ee Bwana.

3. Utujalie upendo wa kweli unaothamini na kuenzi zaidi uhai wa binadamu wenzetu, kuliko kitu kingine chochote. Ee Bwana.

4. Kila mmoja wetu ajibidishe kutafuta mema, wala si mabaya; kwani Wewe hupendezwi na ibada ya unafiki isiyoandamana na matendo mema. Ee Bwana.

5. Uwahurumie wagonjwa, wazee, wageni, yatima, wajane na wote wasiojiweza. Nao marehemu wetu wafikishwe mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyetuamshia mapendo ya kweli, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.



MASOMO YA MISA 1/07/2025

JUMANNE JUMA 13 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.19:15-29
Hata alfajiri ndipo malaika walimhimiza Lutu, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. Akakawia-kawia; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi Bwana alivyohurumia, wakamtoa wakamweka nje ya mji. Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako; usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. Lutu akawaambia, Sivyo, bwana wangu! tazama, mtumwa wako ameona kibali machoni pako, nawe umezidisha rehema zako ulizonifanyia kwa kuponya nafsi yangu, nami siwezi kukimbilia mlimani nisipatwe na yale mabaya, nikafa. Basi mji huu u karibu, niukimbilie, nao ni mdogo, nijiponye sasa huko, sio mdogo huu? Na nafsi yangu itaishi. Akamwambia, Tazama, nimekukubali hata kwa neno hili, kwamba sitauangamiza mji huo uliounena. Hima, ujiponye huko, maana siwezi kufanya neno lo lote, hata uingiapo humo. Kwa hiyo jina la mji ule likaitwa Soari. Jua lilikuwa limechomoza juu ya nchi Lutu alipoingia Soari. Ndipo Bwana akanyesha juu ya Sodoma na juu ya Gomora kiberiti na moto toka mbinguni kwa Bwana. Akaangusha miji hiyo na Bonde lote, na wote waiiokaa katika miji hiyo, na yote yaliyomea katika nchi ile. Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi. Ibrahimu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za Bwana, nave akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuru. Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.26:2-3,9-12 (K)3
1. Ee Bwana, unijaribu na kunipima; Unisafishe mtima wangu na moyo wangu. Maana fadhili zako zi mbele ya macho yangu, Nami nimekwenda katika kweli yako.

(K) Fadhili zako, ee Bwana,
zi mbele ya macho yangu.

2. Usiiondoe nafsi yangu pamoja na wakosaji, Wala uhai wangu pamoja na watu wa damu. Mikononi mwao mna madhara, Na mkono wao wa kuume umejaa rushwa. (K)

3. Ila mimi nitakwenda kwa ukamilifu wangu; Unikomboe, unifanyie fadhili. Mguu wangu umesimama palipo sawa; Katika makusanyiko nifamhimidi Bwana. (K)

SHANGILIO: Yn.14:23
Aleluya, aleluya!
Mtu akinipenda, atalishika neno langu,
na Baba yangu atampenda, na sisi tutakuja kwake.
Aleluya!

INJILI: 
Mt.8:23-27
Yesu alipanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata. Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia. Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu. Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?

MAOMBI
Ndugu, sisi sote tumeitwa kuzishiriki ahadi za ukombozi. Kwa kuwa wokovu wetu unahitaji msaada wa Mungu na maongozi ya malaika, tuombe neema yake.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Kwa maongozi ya malaika wako watakatifu, uwaimarishe viongozi wetu wa Kanisa, ili watekeleze kazi zao za kichungaji hata katika mazingira yenye dhoruba kali. Ee Bwana.

2. Watawala wa dunia wajaliwe kuheshimu haki ya kila mtu kuwa na eneo la makazi, ili kila raia apate mahali pa kulaza kichwa chake. Ee Bwana.

3. Utuepushe na anasa za dunia, kwani husababisha dhambi zinazoamsha hasira yako na kututenga na upendo wako. Ee Bwana.

4. Uzijalie familia zetu mapatano ya kweli; uziepushe na mitego ya yule mwovu na uziweke tayari kuonana nawe muda wowote. Ee Bwana.

5. Malaika wako wawafikishe marehemu wetu kwenye nyumba yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu msamehevu, unayetaka tuyatii maongozi ya malaika wako watakatifu, upokee dua zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 30/06/2025

JUMATATU JUMA 13 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1:
 
Mwa.18:16-33
Watu hao waliondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize. Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu, ili kwamba Bwana naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1-4,8-11 (K)8
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K) Bwana amejaa huruma na neema.

2. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, (K)

3. Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. (K)

4. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. (K)

SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu huisikia sauti yangu;
mimi nawajua, nao hunifuata.
Aleluya!

INJILI: 
Mt.8:18-22
Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

MAOMBI
Kwa vile tunautambua utukufu wa Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli, hatuna budi kumwomba Mungu mwenyewe tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Pokea sala za Baba Mtakatifu, Maaskofu na Mapadre wanazokutolea kwa ajili ya Kanisa lako. Ee Bwana.

2. Uwaonye watu wa mataifa wasiotaka kukukiri Wewe Mungu, wala kuzitubu dhambi zao. Ee Bwana.

3. Utujalie kuitikia mwito wako wa kuitangaza Injili kokote unakotaka, bila kutoa udhuru wala masharti yoyote. Ee Bwana.

4. Kwa huruma yako, utuepushe na dhambi zinazoichafua miili yetu ambayo ni hekalu la Roho wako Mtakatifu. Ee Bwana.

5. Uwapokee ndugu zetu marehemu katika makao yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyewafunulia watakatifu makusudio ya moyo wako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.






MASOMO YA MISA 29/06/2025

WAT. PETRO NA PAULO MITUME

MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA:
Hawa ndio wale, ambao walipoishi, walipanda Kanisa kwa damu yao: walikunywa kikombe cha Bwana, wakawa rafiki zake Mungu.

KOLEKTA:
Ee Mungu, umetujalia tuifurahie siku hii takatifu na tukufu kwa sherehe ya watakatifu Petro na Paulo, mitume. Ulijalie Kanisa lako ili katika mambo yote lifuate maagizo yao, maana kwao limepokea mwanzo wa Ukristo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1:
 Mdo.12:1-11
Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa Kanisa. Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohane, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi, akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi Vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya Watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule Petro alikuwa amelala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-6(K)7
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Malaika wa Bwana hufanya kituo
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.

2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

SOMO 2:
 2Tim.4:6-8,17-18
Mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika. Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda; baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifikie ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina.

SHANGILIO: Mt.16:18
Aleluya, aleluya!
Wewe ndiwe Petro,
na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu;
wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Aleluya!

INJILI:
 Mt.16:13-19
Yesu akaenda pande za Kaisaria Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

MAOMBI
Ndugu wapenzi, Mungu alionesha nguvu ya neema yake alipomwita Petro, mvuvi dhaifu, awe mwamba ambao juu yake alijenga kanisa lake na alimwongoza mdhalimu Saulo awe mhubiri wake mkuu, tukitegemea maombezi yao Tuombe.

Ee Mungu Baba yetu,
1. Ulisaidie Kanisa lako lishikilie imani katoliki ya kitume kwa ajili ya wokovu wa watu wote.

2. Umwangaze na kumwimarisha Baba Mtakatifu katika kazi yake ya kuitetea na kuilinda imani katoliki.

3. Uwaunganishe wakristo wote katika Kanisa moja takatifu la kitume.

4. Uwaongoze wakristo wote wamheshimu Baba Mtakatifu kama wakili wa Kristo hapa duniani.

5. Ufungue mioyo ya wanadamu wote wayaamini mafundisho ya Enjili.

Ee Mungu Mwenyezi wa milele, leo tunaadhimisha sikukuu ya Mitume Petro na Paulo. Hao wamewafundisha wanadamu kumwamini Mungu mmoja na kumheshimu. Sikiliza maombezi yao, ukatupe neema ya kuwa waaminifu siku zote. Kwa Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba, sala ya mitume iandamane na dhabihu tunayokutolea ili itakaswe kwa jina lako; nayo sala itupe uchaji wako tunapokutolea sadaka hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Utume wa Petro na Paulo katika Kanisa.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Kwa maana mitume wako Petro na Paulo kwa mpango wako wanatujalia furaha. Petro alikuwa wa kwanza kukiri imani; na Paulo alieleza imani kwa ufasaha. Petro aliweka misingi ya Kanisa la kwanza kwa mabaki ya wana wa Israeli; Paulo aliitwa awe mwalimu wa Mataifa. Hivyo kwa karama zao mbalimbali waliiunda familia moja ya Kristo, wote wawili wakiheshimiwa duniani kote, wakashiriki taji lililo moja.
Kwa hiyo, sisi pamoja na watakatifu na Malaika Wote tunakutukuza, tukisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Mt.16:16,18
Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kupokea sakramenti hii, utujalie tudumu katika Kanisa, ili, tukiendelea kuumega mkate na kuyashika mafundisho ya mitume, tuwe na moyo mmoja na roho moja, tukiimarishwa kwa upendo wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.










MASOMO YA MISA 28/06/2025

JUMAMOSI JUMA 12 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.18:1-15
Bwana alimtokea lbrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari, Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Nave alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. Basi lbrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. lbrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati uu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi lbrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? Bwana akamwambia lbrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati uu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka.

WIMBO WA KATIKATI: Lk.1:46-50,53-55 (K)54
1. Moyo wangu wamwadhimisha Bwana. Na roho yangu imemfurahia Mungu Mwokozi wangu.

(K) Bwana alikumbuka rehema zake.

2. Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa. (K)

3. Kwa kuwa mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi, Kwa hao wanaomcha. (K)

4. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake: Ili kukumbuka rehema zake. Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele. (K)

SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale walisikio
neno la Bwana na kulishika
Aleluya!

INJILI: 
Mt.8:5–17
Yesu alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, amsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana. Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye. Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli. Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki, na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile. Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwewe Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa. Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia. Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, na kuyachukua magonjwa yetu.

MAOMBI
Ee Mungu, umetufunulia kuwa Wewe upo pia katika nafsi za wenzetu, hasa wale wanaohitaji msaada wetu. Kwa vile si rahisi kuwabaini wenye nia mbaya, twakuomba:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa imani thabiti, wapate kuwaokoa waamini wao dhidi ya yule mwovu, kwa neno lako na kwa kuadhimisha Sakramenti zako. Ee Bwana.

2. Uwajalie wote wenye mamlaka kukuogopa Wewe Mungu, na kuwahudumia walio chini yao kwa utu wema, na hivi kuheshimu uhuru wao na haki za kibinadamu. Ee Bwana.

3. Utuepushe na hila za yule mwovu katika harakati zetu za kutimiza amri ya kukupenda Wewe na jirani. Ee Bwana.

4. Wote wenye shida wasichoke kukukimbilia Wewe kwa sala; na uwajalie mahitaji yao yote. Ee Bwana.

5. Ndugu zetu wagonjwa waponywe kwa jina lako; na marehemu wote watakaswe dhambi zao na kuvikwa utukufu wa ufufuko huko mbinguni. Ee Bwana.

Tunaomba Mama yetu Bikira Maria azisindikize sala zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 27/06/2025

MOYO MTAKATIFU WA YESU MWAKA C

 MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.33:11,19
Makusudi ya Moyo wake ni ya vizazi na vizazi, yeye huwaponya nafsi zao na mauti, na kuwahuisha wakati wa njaa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi, tunaona fahari juu ya Moyo wa Mwanao mpenzi, na kukumbuka fadhili za ajabu za mapendo yake kwetu. Tunakuomba utujalie tustahili kupokea neema tele katika chemchemi hiyo ya karama za mbinguni. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

Au:
Ee Mungu, kwa huruma yako unapenda kutujalia hazina isiyopimika ya upendo katika Moyo wa Mwanao uliojeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu. Tunakuomba utujalie ili, kwa kumtolea heshima ya ibada yetu, tutimize pia wajibu wa malipizi yatupasayo. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1:
 Eze.34:11-16
Bwana Mungu asema hivi: Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu. Nami nitawalisha malisho mema, na juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu nami nitawalaza, asema Bwana Mungu. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.23, (K)1
1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu;
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.

(K) Bwana ndiye mchungaji wangu
Sitapungukiwa na kitu.

2. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaaogopa mabaya;
Kwa maana Wewe upo pamoja nami
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kiombe changu kinafurika. (K)

4. Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

SOMO 2: 
Rum.5:5-11
Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu. Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki, lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Basi Mungu aonesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na gadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya mwana wake, zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumepokea huo upatanisho.

SHANGILIO: Yn.10:14
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi mchungaji mwema;
asema Bwana;
nao walio wangu nawajua;
na walio wangu wanijua mimi;
Aleluya!

INJILI:
 
Lk.15:3-7
Yesu aliwaambia mfano huu, ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aenda akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, Bwana Yesu alijionesha kwetu kama mchungaji mwema anayeacha kondoo tisini na tisa jangwani ili kumtafuta mmoja aliyepotea.

Ee Bwana Yesu,
1. Ulifanya juu chini ili kumpata kondoo mmoja aliyepotea. Utupe matumaini ya kutokuachwa katika shida na utuokoe katika kila hatari.

2. Wewe ulisema kwamba ni mchungaji mwema. Utuzibue masikio yetu ili tusikie sauti yako na kukufuata kama kiongozi katika njia ya kwenda kwa Baba.

3. Unafurahi kuwakaribisha waliopotea na kukurudia. Usituache katika hali ya kukusahau, bali utuhimize kurudi kwako uliye chemchemi ya furaha yetu.

4. Wewe ni mchungaji unayehatarisha maisha yako kwa ajili yetu. Utuwezeshe kukutumaini na kukutegemea daima.

Ee Mungu Baba, Mwana wako alijibidisha sana kutuokoa hata kutoa maisha yake. Ana nia ya kutuchunga tusipotee katika njia ya kufika kwako. Tunaomba hayo kwa njia yake yeye anayeishi na kutawala nawe milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utazame upendo usio na kifani wa Mwanao mpenzi, ili sadaka tunayokutolea ikupendeze na kuwa kwetu fidia ya dhambi zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Mapendo Makuu ya Kristo.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye aliinuliwa msalabani, akajitoa mwenyewe kwa upendo wa ajabu kwa ajili yetu. Alichomwa ubavu, akamwaga damu na maji, zipate kububujika kutoka humo sakramenti za Kanisa, ili wote wavutwe na huo Moyo wazi wa Mwokozi, na kuchota siku zote kwa furaha neema katika chemchemi hiyo ya wokovu.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Watakatifu na Malaika wote tunakutukuza, tukisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.7:37-38
Bwana asema: Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake.

Au: Yn.19:34
Askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, sakramenti hii ya mapendo ituwashie upendo mtakatifu, ambao, kwa kutuvutia daima kwa Mwanao, utufundishe kumtambua yeye katika ndugu zetu. Anayeishi na kutawala milele na milele.


MASOMO YA MISA 26/06/2025

JUMANNE JUMA 10 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
2Kor.1:18–22
Kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Ndiyo na siyo. Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo. Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Krito, na kututia mafuta, ni Mungu, naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.119:129–133,135 (K)135
1. Shuhuda zako ni za ajabu,
Ndiyo maana roho yangu imezishika.
Kufafanusha maneno yako kwatia nuru,
Na kumfahamisha mjinga.

(K) Umwangazie mtumishi wako uso wako.

2. Nalifunua kinywa changu nikatweta,
Maana naliyatamani maagizo yako.
Unigeukie, unirehemu mimi,
Kama iwahusuvyo walipendao jina lako. (K)

3. Uzielekeze hatua zangu kwa neno lako,
Uovu usije ukanimiliki.
Umwangazie mtumishi wako uso wako,
Na kunifundisha amri zako. (K)

Shangilio: Zab.19:18
Aleluya, aleluya.
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Aleluya.

INJILI:
 Mt.5:13-16
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.

MAOMBI
Ee Mungu, huku jeshi la malaika watakatifu likiusifu utukufu wako, twakuomba.

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa wawe chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, ili Wewe Mungu upate kutukuzwa kwa mfano wa maisha yao matakatifu. Ee Bwana.

2. Wote wenye mamlaka katika jamii zetu watoe majibu ya kweli na kwa wakati wa kufaa, ili kuboresha maisha ya watu wako. Ee Bwana.

3. Kila mmoja wetu awajibike kutimiza wajibu wake kiaminifu, na hivi kuwa kama chumvi na nuru ya ulimwengu kwa matendo mema. Ee Bwana.

4. Muujiza aliotendewa mwanamke mjane wa Sarepta utukumbushe daima kuwa kutoa ni moyo, wala siyo utajiri; na kwamba kila mmoja atalipwa kadiri ya matendo yake. Ee Bwana.

5. Uwageukie na uwarehemu marehemu wetu, wapate kuiona nuru yako iangazayo milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu, malaika wako watakatifu waipeleke mbele yako sala yetu hii. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 25/06/2025

JUMATANO JUMA 12 LA MWAKA WA 1

MASOMO

SOMO 1: 
Mwa.15:1-12,17-18
Neno la Bwana likamjia Abrahamu katika njozi, likinena, Usiogope Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana. Abrahamu akasema, Ee Bwana Mungu, utanipa nini, nami naenda zangu hali sina mtoto, na atakayeimiliki nyumba yangu ni huyu Eliezeri, Mdameski? Abramu akasema, Tazama, hukunipa uzao, na mtu aliyezaliwa nyumbani mwangu ndiye mrithi wangu. Nalo neno la Bwana likamjia likinena, Huyu hatakurithi, bali atakayetoka katika viuno vyako ndiye atakayekurithi. Akamleta nje, akasema, Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu. Akamwambia, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi ili uirithi. Akasema, Ee Bwana Mungu nipateje kujua ya kwamba nitairithi? Akamwambia, Unipatie ndama wa miaka mitatu, Na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa. Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akawaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati

WIMBO WA KATIKATI: Zab.105:1-4,6-9 (K)8
1. Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, Wajulisheni watu matendo yake, Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi, Zitafakarini ajabu zake zote.

(K) Bwana analikumbuka agano lake milele.

2. Jisifuni kwa jina lake takatifu, Na ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote. (K)

3. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake; Enyi wana wa Yakobo, wateule wake. Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu; Duniani mwote mna hukumu zake. (K)

Analikumbuka agano lake milele; Neno lile aliloviamuru vizazi elfu. Agano alilofanya na Ibrahimu, uapo wake kwa Isaka. (K)

SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, ee Yerusalemu,
huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!

INJILI:
 Mt.7:15-20
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Jihadharini na manabii wa uwongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuza matunda mazuri. Kila mti usiozaa tunda zuri hukatwa ukatupwa motoni. Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua.

MAOMBI
Ndugu, huku tukikumbuka kuwa sisi ni kama miti ya matunda, tuombe msaada wa Mungu tukisema:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa kumhubiri Kristo Mwanao kwa ufasaha, ili watu wako wasitekwe na manabii wa uwongo. Ee Bwana.

2. Uamshe mioyo ya watawala wa dunia wasiolitukuza jina lako, ili wayashike maagizo yako, na shuhuda zako, na amri zako kwa moyo wote na kwa roho yote. Ee Bwana.

3. Kwa kuwa umetupatia sisi na vizazi vijavyo nchi hii iwe milki yetu pindi tupo hapa duniani, utujalie kuzitumia mali zetu kwa sifa na utukufu wako. Ee Bwana.

4. Umjalie kila mmoja wetu kuzaa matunda mema yaletayo uzima wa milele. Ee Bwana.

5. Marehemu wetu wafikishwe kwenye nchi uliyotuahidia huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tuzae matunda yatakayodumu mpaka uzima wa milele, utujalie hayo tuliyokuomba. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.


MASOMO YA MISA 24/06/2025

 KUZALIWA KWA MT. YOHANE MBATIZAJI

MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Yn.1:6-7: Lk.1:17
Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu, ulimwinua mtakatifu Yohane Mbatizaji awaandae watu amini kwa ajili ya Kristo Bwana. Uwajalie watu wako neema ya furaha za kiroho na uiongoze mioyo ya waamini wote katika njia ya wokovu na amani. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1:
 Isa.49:1-6
Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; Bwana ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha. Akaniambia: Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina Bwana, na thawabu yangu ina Mungu wangu. Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; Zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.139:1-3,13-15(K)14
1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua,
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu,
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.

(K) Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa. Maana wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,

2. Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
Matendo yako ni ya ajabu. (K)

3. Na nafsi yangu yajua sana,
Mifupa yangu haikusitirika kwako,
Nilipoumbwa kwa siri,
Nilipoungwa kwa ustadi pande za chini za nchi. (K)

SOMO 2: 
Mdo.13:22-26
Paulo alisema, Mungu alimwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu Yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu Wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya Kuja kwake. Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake. Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.

SHANGILIO: Lk.1:76
Aleluya, aleluya!
Nawe, mtoto, utaitwa nabii wake Aliye juu,
Kwa maana utatangulia mbele za uso wa Bwana
umtengenezee njia yake.
Aleluya!

INJILI:
 Lk.1:57-66,80
Ikawa, siku za kuzaa kwake Elisabeti zilipotimia, alizaa mtoto mwanamume. Wakasikia jirani zake na jamaa zake ya kwamba Bwana amemwongezea rehema zake, wakafurahi pamoja naye. Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema, La, sivyo; bali ataitwa Yohane, Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo. Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohane. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu Mungu. Wakaingiwa na hofu wote waliokuwa wakikaa karibu nao; na mambo hayo yote yakatangazwa katika nchi yote ya milima milima ya Uyahudi. Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye. Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu rohoni, akakaa majangwani hata siku ya kutokea kwake kwa Israeli.

MAOMBI
Ndugu zangu, Yoane Mbatizaji alimtayarishia Yesu njia, yaani, aliwatayarisha watu kumpokea Masia. Tuombe.

Ee Baba wa mbinguni,
1. Uwaite vijana wawe tayari kuacha yote na kumtumikia Kristo.

2. Utupelekee watangulizi wanaowavuta watu kwa mahubiri na mifano yao.

3. Utusaidie sisi waumini wote kuwa mwanga kwa wote wasiomjua Kristo.

4. Utupe moyo wa kuwa tayari kujitolea kama watangulizi wa wengine kwa ajili ya Kristo.

5. Utujalie kumwona Kristo uso kwa uso siku ya kuitwa naye.

Ee Mungu Mwenyezi, utujulishe kushika kwa moyo wote njia aliyotuonesha Mtakatifu Yoane Mbatizaji. Kwa Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunavileta vipaji hivi altareni pako tunapoadhimisha kwa heshima kuzaliwa kwake Yohane Mbatizaji, aliyetabiri ujio wa Mwokozi wa ulimwengu na akamtambulisha alipokuja. Anayeishi na kutawala milele na milele.

UTANGULIZI: Utume wa Yohane Mbatizaji, Mtangulizi wa Bwana.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo, Bwana wetu.
Tunausifu ukuu wako katika mtakatifu Yohane, Mtangulizi wa huyo Mwanao, ambaye ulimpa heshima ya kuwa mkubwa kati ya wazao Wa wanawake. Yeye alipozaliwa alileta furaha kubwa, na kabla ya kuzaliwa aliushangilia ujio wa wokovu wa wanadamu. Ni yeye peke yake kati ya manabii wote aliyemwonesha kwa watu Mwanakondoo aletaye ukombozi. Pia alimbatiza mwanzilishi mwenyewe wa ubatizo, na kwa namna hiyo maji yanayotiririka yalitakatifuzwa. Hatimaye, kwa kumwaga damu yake, alistahili kumtolea Yesu ushuhuda mkubwa kabisa.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Nguvu za mbinguni, tunakutukuza daima hapa duniani tukisifu bila mwisho adhama yako kwa sauti kuu:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa majeshi.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Lk.1:78
Kwa njia ya rehema za Mungu wetu, mwangaza utokao juu umetufikia.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumeshibishwa katika karamu ya Mwanakondoo wa Mungu. Tunakuomba ili Kanisa lako linalofurahia kuzaliwa kwake mtakatifu Yohane Mbatizaji, aliyeutabiri ujio wake Yesu, limtambue yeye aliye asili ya uzima mpya wa Kanisa. Anayeishi na kutawala milele na milele.





Shajara Yetu © all rights reserved
MKATOIKI KIGANJANI by mitume technologies